Wizara ya Afya ya Yemen imetangaza kuwa watu 6 wameuawa na wengine 26 kujeruhiwa katika shambulio la anga la Marekani kwenye kiwanda kimoja katika mji wa Bani Matar, magharibi mwa San'aa. Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi makali katika maeneo mbalimbali ya Yemen hususan jimbo la Al Hudaydah katika siku za hivi karibuni.
Licha ya mashambulizi hayo, jeshi la Yemen linaendelea kutetea Muqawama na mapambano ya watu wa Palestina huko Gaza, na kwa kutekeleza operesheni za kipekee ambazo hazijawahi kushuhudiwa, limelenga moyo wa utawala ghasibu, meli zinazohusiana na utawala huo na hata meli za kivita za Marekani katika Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, na limetungua ndege 19 za kisasa zisizo na rubani za Marekani.
Jumapili iliyopita pia jeshi la utawala katili wa Israel liliendeleza jinai za kivita kwa kushambulia na kulipua Hospitali ya Kibaptisti katika mji wa Gaza, na kuharibu jengo la mapokezi na huduma za dharura. Hujuma hiyo iliyofanya kwa baraka na himaya kamili ya Marekani, imesababisha kifo cha mtoto mmoja, ambapo wagonjwa na majeruhi walilazimika kulazwa mitaani.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imelaani kitendo cha kulipuliwa hospitali hiyo na kutimuliwa wagonjwa na majeruhi ikikitaja kuwa ni uhalifu mpya wa kivita uliofanywa na jeshi la Israel kwa baraka za Marekani.
Wamarekani waliingia katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa shabaha ya kuuhami na kuusaidia utawala wa Kizayuni wa Israel na kusimamisha operesheni za vikosi vya Muqawama dhidi ya utawala huo, lakini hatua zao hazikuzaa matunda. Kwani, harakati ya Ansarullah ya Yemen na wapigania uhuru wa Palestina wanaendelea kushambulia maeneo muhimu ya utawala huo na meli za kivita za bwana wake, Marekani, licha ya mauaji ya kimbari yanayofanyika huko Gaza.
Kusimama kidete Muqawama wa Palestina huko Gaza na vikosi vya Yemen katika Bahari Nyekundu kunaonyesha kuwa, wanamuqawama wamefanikiwa katika kupeleka mbele malengo yao na kuushambulia utawala wa Kizayuni na Marekani, mshirika mkuu wa utawala huo ghasibu.
Msimamo wa serikali na jeshi la Yemen unaonyesha kuwa, wako tayari kikamilifu kuendelea kukabiliana na utawala wa Kizayuni na Marekani na kwamba kwa kutumia uwezo wao wa kistratijia na kijeshi katika eneo hilo, hawana haja ya kurudi nyuma au kufanya makubaliano na maadui zao.
Mashambulio ya kinyama ya muungano wa Marekani na Wazayuni kwenye maeneo ya raia huko Palestina na Yemen si tu kwamba hayataulazimisha muqawama kurudi nyuma, bali yanazidisha umoja na mshikamano wa vikosi hivyo. Jinai zinazofanywa na jeshi la Marekani na utawala wa Kizayuni huko Yemen na Palestina zitaongeza ufahamu na mwamko wa jamii ya kimataifa, na wanaharakati wa mashirika ya kiraia wataendelea na juhudi zao za kuwafungulia mashtaka wahusika wa mauaji ya halaiki.
Duru mpya ya mashambulizi ya Marekani na Israel ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Mashambulizi hayo hayana tija kwa Marekani na utawala wa Kizayuni, lakini yatapelekea kuwepo umoja mkubwa zaidi baina ya wananchi wa eneo hili katika kuunga mkono muqawama na kulaaniwa jinai za wavamizi katika medani za kieneo na kimataifa.
342/
Your Comment